Skip to main content

Posts

Showing posts from October 3, 2010

Ukila

Ukila kile kichakwe, cha mwenzio usile Ukila wa pupa ‘siwe, pupa nayo ni ndwele Ukila haramu s’tukue, cha mwendo sikitwale Ukila nla halali ‘we, cha chira na usile Usile waja kuamba, ‘kawa kauli nawe Usile ukajigamba, kukila kisichakwe Usile na kwa mafamba, litoe jasho lakwe Usile wala kuramba, na cha hila kisiliwe Kisiliwe cha litima, wasio na uwezo Kisiliwe cha yatima, chao wastahilizo Kisiliwe hata kama, wewe una uwezo Kisiliwe na cha umma, tatapika ulazo Ulazo na kwa ghiliba, huwa sumu mwenzangu, Ulazo na ukashiba, utalipa kwa Mungu Ulazo ziwezo baba, fedha za mwendo chungu Ulazo hata zi’haba, ziwe zako ndu’yangu