Skip to main content

Posts

Showing posts from 2010

yawezekanaje?

Nomba mkanisikiye, kuna jambo lanikaba Mbwene linitatiziye, hapa,kwingine ni haba Yuongoza msimachoye, kama huu sio msiba Niambiye hala, itawezekanaje? Yezekanaje nambiye, kipofu yuwaongoza Wanamfuata wenziye, nyumaye wamfuatiza Iweje mwe machoye, afuate mja weye jiza? Niambiye hala, itawezekanaje? Yuwenda kwenye ndiaye, muendo wa kupapasa Kawa ategemewaye, insi likuki wamfwasa, Kama hawapotezeye, na mawi yakawakusa Niambiye hala itawezekanaje? Wajenda kimwulizaye, ni kupi pa kukwendea? Fi kawapa majibuye, ‘lo! Sioni pa kwendea!” Mjua ndia hijuiye, ije wale wamlungea? Niambiye hala itawezekanaje? Hujaona luja aliye, akitoa hata mwengo Akiita jamaaye, wakatoke zao chengo “mwizi huyu mbueneye”, wakamfuatiya mgongo Nambiye hala, itawezekanaje? Mwizi kufata mwenziye, kuzifuata nyendoze Ameishika simeye, haja ni akamkomeze Wanyofu wafuatiye, na luja yuwaongoze, Nambiye hala, itawezekanaje? Boza kawa ajuaye, akayashika madaraka Mwamuzi kawa ni yeye, mwe’enzi na

Naililia

Naililia kenya, nchi yangu laazizi fuadi yan'tekenya, kuzuwiya siwezi na ajizi sitofanya, kumwomba mwenyezi aiauni kenya, toka kwa wafinyanzi so wema nakukanya, hawano wafinyanzi kwa hila waibinya, na kutiya makunyanzi sao waibambanya, kukuza yao enzi si wema wanasinya, twawajua ni wafyonzi Niya zao si chanya, n'za kuzua machozi wajuzi wajifanya, hawanao ujuzi amwali wakusanya, wazizoa za wizi wala wakitapanya, nasi twala majonzi

Ukila

Ukila kile kichakwe, cha mwenzio usile Ukila wa pupa ‘siwe, pupa nayo ni ndwele Ukila haramu s’tukue, cha mwendo sikitwale Ukila nla halali ‘we, cha chira na usile Usile waja kuamba, ‘kawa kauli nawe Usile ukajigamba, kukila kisichakwe Usile na kwa mafamba, litoe jasho lakwe Usile wala kuramba, na cha hila kisiliwe Kisiliwe cha litima, wasio na uwezo Kisiliwe cha yatima, chao wastahilizo Kisiliwe hata kama, wewe una uwezo Kisiliwe na cha umma, tatapika ulazo Ulazo na kwa ghiliba, huwa sumu mwenzangu, Ulazo na ukashiba, utalipa kwa Mungu Ulazo ziwezo baba, fedha za mwendo chungu Ulazo hata zi’haba, ziwe zako ndu’yangu

Buriani swahiba

Siku pitile ayami, ukumbi sijasimama Sijajitokea mimi, hata kauli kusema Leo najiamba aimi, mbona sitasema lojema! Niutunge na ulimi, n’nene ya yangu mtima Kisema ni fika mimi, nimeipata naima Mola ameshanihami, menikumbuka Karama Kakomesha zangu kemi, kanondolea nakama Ameshanipa mimi, wangu alo pa mtima Ndio ukawa usemi, ninavyompenda wa mtima Nilitasema kwa semi, waja waje kusoma Kuwa sina masghara mi’, nitampenda daima Bure bure siungami, sivyo singesema ‘metujalia we nami, katupa nyota njema Kajaazia na nyemi, na kila lililojema Huba likasibu kumi,nyoyo zikafungama Tupendane kwa ujumi, wala kwa nadama Sa’ wakati mewadiya, wangu mimi kuhama Nenda ughaibuniya, kwa mwaka huu mzima Sivyo nivyodhaniya, kuwa mapenzi huuma kawa tabu kwachaniya, japo kweli ni lazima Nomba hili nijuliya, nakuenzi kwa gharama Hadi muhla wa kuuya, hubetu limesimama Limefurikia ghaya, zaidi ya takadama Kwa sasa buriani mbuya, ni mwiya wa kuchama Hili nakuahidiya, kukupenda kwa da

Kwa kuwa nakupenda

‘Meandika nikujibu, ulouliza mwenzangu Kwelezeto nastahabu, welewe kauli yangu Kupenda nini sababu, umenisaili tangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Na maadamu hu bubu, utashiba jibu langu Kukupenda si ajabu, wan’saliti moyo wangu Mapenzi yaliusibu, kaubwaga wangu wangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Wala sinistaajabu, hikuwa kupenda kwangu Ngejua huba lan’karibu, ngelikaa ange kwa rungu Likija nilidhurubu, lisitwae mtima wangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Navyokupenda habubu, hujapendwa vile tangu Kwangu uli kama shabu, kunitakasa uchungu Kan’ridhie nawe hebu, ukubalie hayangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Hukuwazia ghalibu, fikra tele kwa mafungu Kitamani un’karibu, niwe wako uwe wangu Viate vyako ‘sababu, vilok’zinga ja magugu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Hujui ngapi hesabu, n’mejipinda   pali mvungu N’kililia lako jibu, litalon’toa kiwingu Uwele likanitibu, mato yao

Raha ina karaha

Nisikiye muandani, hili langu ‘takufaa Likulinde maishani, upate na manufaa Usikimbilie rahani, si kwote kwa shufaa Raha siyo ya furaha, mbambonimwe mna karaha Raha haiji kisolo, huja imepachana Unalodhania silo, huwa limepindana Unapolipata hilo, na jingine wakutana Siirambitie raha, mbambonimwe mna karaha Maumbile yakufunze, yana mfano murua Kwanza mulima uanze, pindi bonde tagundua Au mchana na nuruze, usiku utazipindua Ukisha icheza zeze, simile kwaja simanzi Husikii usesikiya, upate na uelewa Wazee ‘lijisemeya, ja bakuli na kawa Raha ukifurahiya, karaha hitachelewa Mwana  ukaindhari, baada ya raha karaha Uchovyapo na asali, usiwe mwenye pupa sana Na utamu wa asali, kuna nyuki na usena Sasa uki si wa azali, una sumu ya usena Na dunia k’ikumbata, kajikaliye yahiyatu Tamati nimeifika, sina mengi ya kunena Sipende kukaramka, ukakosa indhana Raha simfanye kaka, rafiki wa kupendana Mbona usena wa nyuki, nao huo si usena?

Tulikotoka!(limetafsiwa)

Huko tulikotoka!! Japo hakuna umbo wala sura Lakini kulituunda na kutupa sura Japo wengi walilemazwa na kuachwa vichwara Waliofahamu ngomani walisowera Na umbali huu wajisukuma Japo huenda kusizue tamaa Na wengi waweza kupuuza Lakini twakuonea fahari tunavyoweza Tukijua  kumetupa na jina Tulitoa machozi na bila raghba Sasa twavuna naima tukiimba Na hivyo tunamwadhimisha Yeye Aliyetutia nguvu japo wanyonge tuwiliye Sasa twakuonea fahari tulikotoka!! Rejea, tazama na usailie Utaona hakuna kitu ukifurahie Na ukute kuwa hapana kitu kiwilie Ulitima wake ulishamirie Nusura kinamasini tuzamie Lakini hatukutamauka tusishikilie Kwa tumaini la ng’ambo litusubirie Tukaipuuza njaa ilishadidie Kwani nyoyo na nafsi zetu zilipanie Wala zisitamauke na pale ziangukie. Tumaini! Tumaini ndo nanga ilitushikilie Tumaini la kesho itutadhayalie ….Na leo! Twatazama jana toka hapa tufikie Twakutabasamia kwa fahari tulikotokea

Where we came from

Where we came from!! Though it'd no shape nor form, but it defined us n gave us form Though some were disabled and left maim those who understood played the game and thus far they have come Though undesirable it may seem and many may assume but we proudly admire the same Knowing well it made us a name We shed tears and having no whim yet we reap with joy with a hymn and thus credit we give to Him who strengthened us though weak we seem Now we feel proud of where we came from!!! Go back, look and inquire You’ll see nothing to desire And find that nothing was there The need thereof was so dire That we almost sank like in mire But we didn’t give up either For the hope of the awaiting joy yonder We defied the prevailing hunger For our hearts and souls were so eager Not to despair and fall thither Hope! …Hope was our anchor Hope of a tomorrow that would be better…. …And today! We can look back from hither And smile with pride of where we came from

Yupi mwenye haki

1.           Yupi ale mahuluki, asiye kuwa na doa Ni yupi ale na haki, asiye wa kukosoa Mja ambaye hakiuki, akawa wa kupotea Hayupo muenye haki, maki wote meondoa 2.           Yupi asiye wa kosa, mnyofu wazo nyendo, Awapo aseme sasa, akajinegee kando, Yule ale jitakasa, safi hanao uvundo Hakuna asiyekosa, kwa kauli na matendo 3.           Sijaona aliyejitosha, akahimili nafsiye Insi asejikunguisha, ulimi kwa kauliye Nani asiye keresha, kubughudhi muumbaye Ila tu akajikosha, akatubia dhambiye 4.           Nani asiyekunguwaa, kwa fikra ya moyoni Kunaye asiye na waa, lilofichama wazoni? Awe mja anayefaa, kwa Rabana machoni? Wote wamepunguwaa, utukufu hawaoni.   5.           Yupi basi wa kupona? amchaye Mola wake Nani atakayemwona? Asafiye nafsi yake, Mja yupi atayefana? Aseficha ila zake, Amwombaye Rabana, njia zake zinyoke

Mchunguze vizuri

Leo tamwona mwovu, amenawiri Apataye kwa kiwavu,ndiye tajiri Nawe uliye mnyovu, unayo shari Chunga sikwingiye wivu, wewe subiri Ajitendaye manguvu, na takaburi Mchunguze vizuri Kesho iatakudhihiri, ametoweka Mtu yule aliyejibari, katononoka Yamemkuta ya shari, ‘kaporomoka Utafute kwa indhari, nayo hakika Hutomwona nayo kheri, ameondoka Mchunguze vizuri   Miye huyu nakweleze, yalo ya kweli Zimefupishwa sikuze,haendi mbali Mola ajua insize, k’watajamali Ampa njema sikuze, mustakabali Mwovu mali si malize, muhifadhili Mchunguze vizuri Asema wazi mwenyezi, kitabunimwe Mjawe kumwacha hawezi, hatupwi kamwe Waovu tawaweka wazi, shetani pamwe Na wanyofu awajazi, wahifadhiwe Wovu wadhili kwa kazi, wakufaidiwe Mchunguze vizuri