Skip to main content

Posts

Showing posts from September 19, 2010

Kwa kuwa nakupenda

‘Meandika nikujibu, ulouliza mwenzangu Kwelezeto nastahabu, welewe kauli yangu Kupenda nini sababu, umenisaili tangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Na maadamu hu bubu, utashiba jibu langu Kukupenda si ajabu, wan’saliti moyo wangu Mapenzi yaliusibu, kaubwaga wangu wangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Wala sinistaajabu, hikuwa kupenda kwangu Ngejua huba lan’karibu, ngelikaa ange kwa rungu Likija nilidhurubu, lisitwae mtima wangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Navyokupenda habubu, hujapendwa vile tangu Kwangu uli kama shabu, kunitakasa uchungu Kan’ridhie nawe hebu, ukubalie hayangu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Hukuwazia ghalibu, fikra tele kwa mafungu Kitamani un’karibu, niwe wako uwe wangu Viate vyako ‘sababu, vilok’zinga ja magugu Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda Hujui ngapi hesabu, n’mejipinda   pali mvungu N’kililia lako jibu, litalon’toa kiwingu Uwele likanitibu, mato yao

Raha ina karaha

Nisikiye muandani, hili langu ‘takufaa Likulinde maishani, upate na manufaa Usikimbilie rahani, si kwote kwa shufaa Raha siyo ya furaha, mbambonimwe mna karaha Raha haiji kisolo, huja imepachana Unalodhania silo, huwa limepindana Unapolipata hilo, na jingine wakutana Siirambitie raha, mbambonimwe mna karaha Maumbile yakufunze, yana mfano murua Kwanza mulima uanze, pindi bonde tagundua Au mchana na nuruze, usiku utazipindua Ukisha icheza zeze, simile kwaja simanzi Husikii usesikiya, upate na uelewa Wazee ‘lijisemeya, ja bakuli na kawa Raha ukifurahiya, karaha hitachelewa Mwana  ukaindhari, baada ya raha karaha Uchovyapo na asali, usiwe mwenye pupa sana Na utamu wa asali, kuna nyuki na usena Sasa uki si wa azali, una sumu ya usena Na dunia k’ikumbata, kajikaliye yahiyatu Tamati nimeifika, sina mengi ya kunena Sipende kukaramka, ukakosa indhana Raha simfanye kaka, rafiki wa kupendana Mbona usena wa nyuki, nao huo si usena?

Tulikotoka!(limetafsiwa)

Huko tulikotoka!! Japo hakuna umbo wala sura Lakini kulituunda na kutupa sura Japo wengi walilemazwa na kuachwa vichwara Waliofahamu ngomani walisowera Na umbali huu wajisukuma Japo huenda kusizue tamaa Na wengi waweza kupuuza Lakini twakuonea fahari tunavyoweza Tukijua  kumetupa na jina Tulitoa machozi na bila raghba Sasa twavuna naima tukiimba Na hivyo tunamwadhimisha Yeye Aliyetutia nguvu japo wanyonge tuwiliye Sasa twakuonea fahari tulikotoka!! Rejea, tazama na usailie Utaona hakuna kitu ukifurahie Na ukute kuwa hapana kitu kiwilie Ulitima wake ulishamirie Nusura kinamasini tuzamie Lakini hatukutamauka tusishikilie Kwa tumaini la ng’ambo litusubirie Tukaipuuza njaa ilishadidie Kwani nyoyo na nafsi zetu zilipanie Wala zisitamauke na pale ziangukie. Tumaini! Tumaini ndo nanga ilitushikilie Tumaini la kesho itutadhayalie ….Na leo! Twatazama jana toka hapa tufikie Twakutabasamia kwa fahari tulikotokea

Where we came from

Where we came from!! Though it'd no shape nor form, but it defined us n gave us form Though some were disabled and left maim those who understood played the game and thus far they have come Though undesirable it may seem and many may assume but we proudly admire the same Knowing well it made us a name We shed tears and having no whim yet we reap with joy with a hymn and thus credit we give to Him who strengthened us though weak we seem Now we feel proud of where we came from!!! Go back, look and inquire You’ll see nothing to desire And find that nothing was there The need thereof was so dire That we almost sank like in mire But we didn’t give up either For the hope of the awaiting joy yonder We defied the prevailing hunger For our hearts and souls were so eager Not to despair and fall thither Hope! …Hope was our anchor Hope of a tomorrow that would be better…. …And today! We can look back from hither And smile with pride of where we came from

Yupi mwenye haki

1.           Yupi ale mahuluki, asiye kuwa na doa Ni yupi ale na haki, asiye wa kukosoa Mja ambaye hakiuki, akawa wa kupotea Hayupo muenye haki, maki wote meondoa 2.           Yupi asiye wa kosa, mnyofu wazo nyendo, Awapo aseme sasa, akajinegee kando, Yule ale jitakasa, safi hanao uvundo Hakuna asiyekosa, kwa kauli na matendo 3.           Sijaona aliyejitosha, akahimili nafsiye Insi asejikunguisha, ulimi kwa kauliye Nani asiye keresha, kubughudhi muumbaye Ila tu akajikosha, akatubia dhambiye 4.           Nani asiyekunguwaa, kwa fikra ya moyoni Kunaye asiye na waa, lilofichama wazoni? Awe mja anayefaa, kwa Rabana machoni? Wote wamepunguwaa, utukufu hawaoni.   5.           Yupi basi wa kupona? amchaye Mola wake Nani atakayemwona? Asafiye nafsi yake, Mja yupi atayefana? Aseficha ila zake, Amwombaye Rabana, njia zake zinyoke

Mchunguze vizuri

Leo tamwona mwovu, amenawiri Apataye kwa kiwavu,ndiye tajiri Nawe uliye mnyovu, unayo shari Chunga sikwingiye wivu, wewe subiri Ajitendaye manguvu, na takaburi Mchunguze vizuri Kesho iatakudhihiri, ametoweka Mtu yule aliyejibari, katononoka Yamemkuta ya shari, ‘kaporomoka Utafute kwa indhari, nayo hakika Hutomwona nayo kheri, ameondoka Mchunguze vizuri   Miye huyu nakweleze, yalo ya kweli Zimefupishwa sikuze,haendi mbali Mola ajua insize, k’watajamali Ampa njema sikuze, mustakabali Mwovu mali si malize, muhifadhili Mchunguze vizuri Asema wazi mwenyezi, kitabunimwe Mjawe kumwacha hawezi, hatupwi kamwe Waovu tawaweka wazi, shetani pamwe Na wanyofu awajazi, wahifadhiwe Wovu wadhili kwa kazi, wakufaidiwe Mchunguze vizuri