Skip to main content

Posts

Showing posts from February 3, 2013

Kenya Itakuwepo

Niskize kote mlipo, niwape huno ujuzi Siku ya kura ijapo, ‘kiteuwa viongozi Kabila zetu zingapo, nyingi baidi ki’zazi Tutunze kenya iwepo, baada ya uchaguzi Na siasa tupigapo, tusitiye machokozi, kila mwahala twendapo, tudhihirishe wongozi, na wala sio matapo, ya kuzua machukizi, Hi' kenya itakuwapo, baada ya uchaguzi. Wazi mwajuwa malipo, ya kuzua uchafuzi, na kujifanya mapopo, tusiyatie maozi, ela yatendwe tulipo, wengi kawa wakimbizi, twataka kenya iwepo, baada ya uchaguzi kataa vidingapopo, vya kuzua uchochezi nao hawatakuwapo, tukichomana kwa mionzi wakipoa kwao pepo, nasi twazipiga kwenzi tuombe Kenya iwepo, baada ya uchaguzi Sisemi kupita hapo, menikaba usingizi, na chini nijilazapo, nawaasa wasikizi, kila mwahala mlipo, tusirudiye ya juzi, ili kenya ikawepo, baada ya uchaguzi. K.W Wamalwa Mlokole Mlumbi Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison