Skip to main content

Posts

Showing posts from April 10, 2011

Wangu ulojisunda

Nudhumu ninaiunda, ya mtimani kukuamba Yakufike ulikowanda, ujue yanonikumba Ninakwita uloenda, mbali ulikotamba Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda Kufikiri nimeshinda, nazuzuika ja mshamba Sikwachi kukupenda, hata nizinge kwa ndumba Suhuba imenitanda, nisikiye nakuomba Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda Fuadi imekuganda, hibanduki kama gamba Kama maua ya nyanda, imeshachanua tumba Ndo sikomi kukuwinda, na tungo nikilumba Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda Mwendo naziuma zanda, kwa kukukosa mchumba Atiati yanipanda, nawazia kwenda kamba Nishaifikia kenda, kama kuhesabu namba Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda