Skip to main content

Posts

Showing posts from July 24, 2011

Yana wenyewe

Makonde ya usuhuba, hayo yanao wenyewe Yanataka waloshiba, wakapandwa na viwewe Aimi wa nguvuhaba! sezi viwavu n'waniwe Huba ni la wa manguvu, n'lokifyefye najitowa N'lokifyefye najitowa, niachiye wenye nguvu Sitwai ningapawa, nachia yangu makovu Kumbe hayanayo dawa, yenye  kuleta utuvu Vikumbo vyayo mapenzi, vyahitaji wenye navyo Vyahitaji wenye navyo, wanotumia ja vyambo, Ukicheza nao ovyo, hutohimili makumbo Walai mja mimi sivyo, lau n'katowa matumbo Masumbwi ya huba n'yao, wenye mbinu za mikono Wenye mbinu za mikono, wajitenda pasi indha Wajuzi wa mavongono, hini kwao ndio ladha Kwazo kucha na vijino, wamewaatua kadha Mafundo yayo mahaba, ni ya wale wasimoyo Ni ya wale wasimoyo, walotasa wa hisia Ndio walo na   uchoyo, waja wanojitakia Huwezi ngapiga mbio, au kilema takutia Una kani chache flani, kana uwachie wao Kana uwachie wao, nakwamba ni wachokozi Kila kito ni cha kwao, sivyo wakulize chozi Nawajua watu zao, mbwene na yangu maozi