Skip to main content

Posts

Showing posts from May 1, 2011

Bin-Adamu

Mimi Natakadamu ino nudhumu Nikayaambe yalomuhimu Yanotaja ghilba za bin-Adamu Wa kuhalalisha yalokharamu kufaidi yake tamaa na hamumu Yalo mema kayatiya sumu Na kuwaseta walomaamumu Wakijigeuza sanamu Wakisahau wali wanadamu Kataka ibada kwa kaumu Wadhani Takwepa luhdi wakisha humu Watakinza ya Mungu Kalamu Kwamba Muhuluku hafahamu ati hiyeyuki fuadi ngumu Ila Wendelepi siku ya hukumu? Watapokwima mbele ya Hakimu Kulipiya wao udhalimu Kama si nyoto za Jehanamu? Zitakao waunguza kwa zamu Zikisha lamba mifupa na damu Watauma zanda na kujilaumu kwa wao utimamu wa wazimu ©Wamalwa
Naja kwa jina lake Mungu Kwamba yalo moyoni mwangu Yaliyo tamu na machungu Uje kulimuka mwenzangu Ukituliana nikwambie Nitasema pasi kificha Nikuonye bila kukucha Kuwa jambo ‘kikufikicha La ukweli uliochacha Nihisani uniambie Hakuna aliyenyooka Muenda asiyeteguka Kwa wazo au kutamuka Miye pia wakupunguka Ukiona ila nambie Ni wa chira asoonyeka Muambae asokanyika Mara tatu hajaambika Atajuta akikutika Zamu yako ni umwambie Ukweli mchungu huuma Na hugharimu kuusema Ela ni dawa ya hatima Huja kuuponya mtima Ukiwa nao   we’nambie Kanyo lako ukichelea Ukiniona nakosea Kwa Mungu ukijitetea Hesabu utanitolea Kujitoa ila,nambie Niambie liwapo chungu Usinifumbie mizungu Walau likawe uchengu Mwanga wa maozi yangu Usiche kuindha nambie Natua hapa nikuindha Kwa hayo maonyo kadha Kuyashika kwako faradha Maishani yakupe ladha Ela hikufai, nambie © Wamalwa

Ningekwambia!

Kama ingekuwa vile, swahiba ningeshasema Ningepiga na kelele, ufahamu himahima Kwamba sikuwazi miye, sikomi laili nzima Ningejasiri n’kwambie, lau sikupendi mbuya Kama sivyo ‘ngekwambiya, wazi wazi pasi siri Lau sijasuhubiya, nahari sikufikiri Kwamba sijakuwaziya, na gonezi kuabiri Ngaungama wangu mwari, kwamba siwe nimpendaye Kama kuli mwengineye, ninaye muenendea Mtimangu anitwaliye, ni radhi kumwenendea Hadhi yangu nimpaye, na siwe wangu maridia Ngakwambia siweye, hala ningekuhubiri Kama siwe ulinitwaa, kawa wa kunipa tuo Najenenda nili fwaa, nimetekwa na pumbao Azizi u’vyonivaa, yakaniisha matao Kweli ningeshakujuza, kwamba siwe nyonda

Nikome Uniambae

Kama utanisikiya, nambe haya kukuindha Majambo nilowaziya, si moja ila ni kadha Yenye heri kufaidiya, ungayafwata faradha Kama sivyo swahibiya, nikome nambae Kama uli wa kukimbiya, na haraka za vitendo, Naona huton’faiya, zangu ni   za pole nyendo Mambo mi’ hiyapaniya, haraka ina uvundo Kama hutosubiriya, nikome uniambae Kama limi umenoya, linakata kama msu Na Inda   kutapakaya, ndugu kuwagawa nusu Nyoyo kuwakereya, na kukeeza ja kisu Kama ndugu kuchukiya, nikome uniambae Kama huli wakupenda, umejaa inda na inadi Chuki imejenga banda, imekingama f uadi Sin’tiye kwayo mawanda, naona umeshadidi Kama hutogeukiya, nikome uniambae