Skip to main content

Yana wenyewe

Makonde ya usuhuba, hayo yanao wenyewe
Yanataka waloshiba, wakapandwa na viwewe
Aimi wa nguvuhaba! sezi viwavu n'waniwe
Huba ni la wa manguvu, n'lokifyefye najitowa

N'lokifyefye najitowa, niachiye wenye nguvu
Sitwai ningapawa, nachia yangu makovu
Kumbe hayanayo dawa, yenye  kuleta utuvu
Vikumbo vyayo mapenzi, vyahitaji wenye navyo

Vyahitaji wenye navyo, wanotumia ja vyambo,
Ukicheza nao ovyo, hutohimili makumbo
Walai mja mimi sivyo, lau n'katowa matumbo
Masumbwi ya huba n'yao, wenye mbinu za mikono

Wenye mbinu za mikono, wajitenda pasi indha
Wajuzi wa mavongono, hini kwao ndio ladha
Kwazo kucha na vijino, wamewaatua kadha
Mafundo yayo mahaba, ni ya wale wasimoyo

Ni ya wale wasimoyo, walotasa wa hisia
Ndio walo na  uchoyo, waja wanojitakia
Huwezi ngapiga mbio, au kilema takutia
Una kani chache flani, kana uwachie wao

Kana uwachie wao, nakwamba ni wachokozi
Kila kito ni cha kwao, sivyo wakulize chozi
Nawajua watu zao, mbwene na yangu maozi
Bahari’no ya  mapenzi, ina papa wavumao

Ina papa wavumao, havipezi vikambare
Nashusha yangu matao, nepuke zao ndarire
Wanayo satua yao, ninawacha wasowere
Mikwato ya suhubani, ina hao masogora

Ina hao masogora, wasojuwa na hisani,
Ndio waja wenye chira, kupoka kwao ndo shani
Hawachi k’leta khasara, kuwatenga wendani
Hila zilo mapenzini, Walai zina wenyewe


Wamalwa K.W
Mlokole Mlumbi
Kamukuywa






Comments

Popular posts from this blog

Mja hafi kupenda

Hapana mja duniani, apenda aondowe Si khiari asilani, rohoye aitowe Aingiye pa gizani, kusiko na mwendowe Maja hafi kupenda, n’ kudura itimiye Ni kudura ya Manani, alompa utuwe Hana na lake Fulani, sema akohowe Hanalo la lakini, zake ziandikiwe Mja hafi kupenda, n’kudura itimiye          Nyaka zikiwa shirini,ni jaala apawe Au aishi theneni, neema ajaliwe Mja hana kwa nini,ikiwa aitiwe Mja hafi kupenda,n’ kudura itimiye Lau ngapewa idhini, k’teuwa atakaye Ngebaki duniani, amwali ajiliye   Afurahi maishani, na wale wampendaye Mja hafi kupenda , n’kudura itimiye

Yupi mwenye haki

1.           Yupi ale mahuluki, asiye kuwa na doa Ni yupi ale na haki, asiye wa kukosoa Mja ambaye hakiuki, akawa wa kupotea Hayupo muenye haki, maki wote meondoa 2.           Yupi asiye wa kosa, mnyofu wazo nyendo, Awapo aseme sasa, akajinegee kando, Yule ale jitakasa, safi hanao uvundo Hakuna asiyekosa, kwa kauli na matendo 3.           Sijaona aliyejitosha, akahimili nafsiye Insi asejikunguisha, ulimi kwa kauliye Nani asiye keresha, kubughudhi muumbaye Ila tu akajikosha, akatubia dhambiye 4.           Nani asiyekunguwaa, kwa fikra ya moyoni Kunaye asiye na waa, lilofichama wazoni? Awe mja anayefaa, kwa Rabana machoni? Wote wamepunguwaa, utukufu hawaoni.   5.           Yupi basi wa kupona? amchaye Mola wake Nani ataka...