Yakufike ulikowanda, ujue yanonikumba
Ninakwita uloenda, mbali ulikotamba
Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda
Kufikiri nimeshinda, nazuzuika ja mshamba
Sikwachi kukupenda, hata nizinge kwa ndumba
Suhuba imenitanda, nisikiye nakuomba
Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda
Fuadi imekuganda, hibanduki kama gamba
Kama maua ya nyanda, imeshachanua tumba
Ndo sikomi kukuwinda, na tungo nikilumba
Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda
Mwendo naziuma zanda, kwa kukukosa mchumba
Atiati yanipanda, nawazia kwenda kamba
Nishaifikia kenda, kama kuhesabu namba
Jifaraghua e nyonda, wangu uliyejisunda
Comments