Siku pitile ayami, ukumbi sijasimama
Sijajitokea mimi, hata kauli kusema
Leo najiamba aimi, mbona sitasema lojema!
Niutunge na ulimi, n’nene ya yangu mtima
Kisema ni fika mimi, nimeipata naima
Mola ameshanihami, menikumbuka Karama
Kakomesha zangu kemi, kanondolea nakama
Ameshanipa mimi, wangu alo pa mtima
Ndio ukawa usemi, ninavyompenda Nelima
Nilitasema kwa semi, waja waje kusoma
Kuwa sina masghara mi’, nitampenda daima
Bure bure siungami, sivyo singesema
‘metujalia we nami, katupa nyota njema
Kajaazia na nyemi, na kila lililojema
Huba likasibu kumi,nyoyo zikafungama
Tupendane kwa ujumi, wala kwa nadama
Sa’ wakati mewadiya, wangu mimi kuhama
Nenda ughaibuniya, kwa mwaka huu mzima
Sivyo nivyodhaniya, kuwa mapenzi huuma
kawa tabu kwachaniya, japo kweli ni lazima
Nomba hili nijuliya, nakuenzi kwa gharama
Hadi muhla wa kuuya, hubetu limesimama
Limefurikia ghaya, zaidi ya takadama
Kwa sasa buriani mbuya, ni mwiya wa kuchama
Hili nakuahidiya, kukupenda kwa daima
Nalo ninashikiliya, kwa nayo mawi na mema
indi tu nitarejeya, hiyo yetu siku njema
Buriani wangu swahiya, Mola tujalie uzima
Hapa nakamiliya, mwisho n’tiye kaditama
Kama nivyosuhubiya, ndivyo hivyo daima
Kama nivyosuhubiya, ndivyo hivyo daima
Nakutakia afiya, ya mwili nao mtima
Hadi twonane mbuya, n’kirejea na salama.
Comments