Skip to main content

Mwana nakuasa


Leo nimekuita mwana,
Nikupe yangu ya moyo
Kwa upole nitanena
‘Kayatiye masikiyo
Tabiya hii yako mwana
Si yetu tujuwayo

Uli wa kulaza damu
Na uzembe uzidiyo
Pahala nawe hudumu
Uchao ni mbiyombiyo
Hutufai nawe humu
Na hiyo shambiroyo

Wapendani naumi
Unaiizia gange
Hulimi na walimi
Wataka ukajitenge
Haya sijaona mimi
Nakuasa ujichunge

Mwiza kazi yu wa chira
Ni aendewaye tenge
Asiyetaka ajira
Wala hashiki shilange
Ndiye muja wa hasara
Hubomoa asijenge

Unavitaka vya bure
Hulitoi jasho lako
Lako ndizo hamrere
Umebaki wa mitiko
Uchao ‘wa’tuza bure
Sizo zetu nyendo zako

La mno lako ni ung’are
Uzirembe nyele zako
Uturi ujirashire
Ukatembee kwa deko
Hukosi kuzua ghere
Na marashi ya mnuko


Unazani utaoa?
Utamwoa wa nani?
Jasho nalo hujatoa,
Utachokishika nini?
Utaithibiti ndoa?
Wa kukubali nani?

Unafaa kujitoa,
Fanye kazi kwa manani
Na mali ukayazoa
Hamadi kibindoni
Ndipo utapopoa
Ukamtafute mwendani

Si mambo ya kutanga
Fi na huyu fi na yule
Chunga utajikaanga
Ati umetujile uwele
Mchumba chumbiya mwenga
Na yule ukamuole

Utafanyani kiwatunga,
Himila wakahimile
Na hilo likawe janga
Na lije likulemele
Mwanangu hutochenga
Wote wakikujile

Kisomo ndiyo unacho
Shahada umejitwaliya
Ujuzi unao kocho
Hutaki kuutumiya
Upate ukitakacho
Kile cha kukufaiya

Mwana wan’tiya kichocho
Kwona umejiachiya
Umekuwa kitumiwacho
Kidhani wawatumiya
Unawapa wapendacho
Nawanachokutakiya

Koma mwanangu ukome
Usinifishe mvyeleo
Usombombi uukome
Ukome kwanzia leo
Sitakwita te’niseme
Ishapita hii leo

Ukware si kuwa dume
Dume ni ajiwekeo
Wa sitaha ndiye dume
Anakheshimu nafseo
Muungwana kama kimeme
Fikiri nokwelezeo

Mradi unayo masikizi,
Haya umenisikiya
Kazituwe nyendo hizi
Ukawe wa kutuliya
Ukasuhubiye kazi
Halafu itakufaiya

Nakoma zaidi s’ezi
Yametosha mekwambiya
Nimekuweko na juzi
Miyaka menipitiya
Nimejizolea ujuzi
Ndiyo ya’ nakupa yaya

Comments

Popular posts from this blog

Mja hafi kupenda

Hapana mja duniani, apenda aondowe Si khiari asilani, rohoye aitowe Aingiye pa gizani, kusiko na mwendowe Maja hafi kupenda, n’ kudura itimiye Ni kudura ya Manani, alompa utuwe Hana na lake Fulani, sema akohowe Hanalo la lakini, zake ziandikiwe Mja hafi kupenda, n’kudura itimiye          Nyaka zikiwa shirini,ni jaala apawe Au aishi theneni, neema ajaliwe Mja hana kwa nini,ikiwa aitiwe Mja hafi kupenda,n’ kudura itimiye Lau ngapewa idhini, k’teuwa atakaye Ngebaki duniani, amwali ajiliye   Afurahi maishani, na wale wampendaye Mja hafi kupenda , n’kudura itimiye

Yupi mwenye haki

1.           Yupi ale mahuluki, asiye kuwa na doa Ni yupi ale na haki, asiye wa kukosoa Mja ambaye hakiuki, akawa wa kupotea Hayupo muenye haki, maki wote meondoa 2.           Yupi asiye wa kosa, mnyofu wazo nyendo, Awapo aseme sasa, akajinegee kando, Yule ale jitakasa, safi hanao uvundo Hakuna asiyekosa, kwa kauli na matendo 3.           Sijaona aliyejitosha, akahimili nafsiye Insi asejikunguisha, ulimi kwa kauliye Nani asiye keresha, kubughudhi muumbaye Ila tu akajikosha, akatubia dhambiye 4.           Nani asiyekunguwaa, kwa fikra ya moyoni Kunaye asiye na waa, lilofichama wazoni? Awe mja anayefaa, kwa Rabana machoni? Wote wamepunguwaa, utukufu hawaoni.   5.           Yupi basi wa kupona? amchaye Mola wake Nani ataka...