Skip to main content
Naja kwa jina lake Mungu
Kwamba yalo moyoni mwangu
Yaliyo tamu na machungu
Uje kulimuka mwenzangu
Ukituliana nikwambie

Nitasema pasi kificha
Nikuonye bila kukucha
Kuwa jambo ‘kikufikicha
La ukweli uliochacha
Nihisani uniambie

Hakuna aliyenyooka
Muenda asiyeteguka
Kwa wazo au kutamuka
Miye pia wakupunguka
Ukiona ila nambie

Ni wa chira asoonyeka
Muambae asokanyika
Mara tatu hajaambika
Atajuta akikutika
Zamu yako ni umwambie

Ukweli mchungu huuma
Na hugharimu kuusema
Ela ni dawa ya hatima
Huja kuuponya mtima
Ukiwa nao  we’nambie

Kanyo lako ukichelea
Ukiniona nakosea
Kwa Mungu ukijitetea
Hesabu utanitolea
Kujitoa ila,nambie

Niambie liwapo chungu
Usinifumbie mizungu
Walau likawe uchengu
Mwanga wa maozi yangu
Usiche kuindha nambie

Natua hapa nikuindha
Kwa hayo maonyo kadha
Kuyashika kwako faradha
Maishani yakupe ladha
Ela hikufai, nambie

©Wamalwa

Comments

Popular posts from this blog

Bin-Adamu

Mimi Natakadamu ino nudhumu Nikayaambe yalomuhimu Yanotaja ghilba za bin-Adamu Wa kuhalalisha yalokharamu kufaidi yake tamaa na hamumu Yalo mema kayatiya sumu Na kuwaseta walomaamumu Wakijigeuza sanamu Wakisahau wali wanadamu Kataka ibada kwa kaumu Wadhani Takwepa luhdi wakisha humu Watakinza ya Mungu Kalamu Kwamba Muhuluku hafahamu ati hiyeyuki fuadi ngumu Ila Wendelepi siku ya hukumu? Watapokwima mbele ya Hakimu Kulipiya wao udhalimu Kama si nyoto za Jehanamu? Zitakao waunguza kwa zamu Zikisha lamba mifupa na damu Watauma zanda na kujilaumu kwa wao utimamu wa wazimu ©Wamalwa

Ukila

Ukila kile kichakwe, cha mwenzio usile Ukila wa pupa ‘siwe, pupa nayo ni ndwele Ukila haramu s’tukue, cha mwendo sikitwale Ukila nla halali ‘we, cha chira na usile Usile waja kuamba, ‘kawa kauli nawe Usile ukajigamba, kukila kisichakwe Usile na kwa mafamba, litoe jasho lakwe Usile wala kuramba, na cha hila kisiliwe Kisiliwe cha litima, wasio na uwezo Kisiliwe cha yatima, chao wastahilizo Kisiliwe hata kama, wewe una uwezo Kisiliwe na cha umma, tatapika ulazo Ulazo na kwa ghiliba, huwa sumu mwenzangu, Ulazo na ukashiba, utalipa kwa Mungu Ulazo ziwezo baba, fedha za mwendo chungu Ulazo hata zi’haba, ziwe zako ndu’yangu

Siku ya Ulifi

Toka Hegi yasikika, imelia parapanda Wafike walotajika, wasilimatie kwenda Majina waliandika, na ila walizotenda Waache kuhemeka, ili siku ya ulifi Nawaasa wahusika, waziache propaganda Hifai kulalamika, kila wanakokuenda Wengine tope kupaka, jukwaani wakipanda Wakuache kupayuka, ili siku ya ulifi Wenyewe waliyataka, mbegu mbaya walipanda Na chuki waliipika, ikaiva na kuvunda Na Umma ukagawika, maovu ukajitenda Sasa wana jakajaka, ili siku ya ulifi Mahuluki bila shaka, huvuna ‘lichopanda Na maji ukiyateka, uyanywe yote mafunda Na koo ikikabika, shauriyo ‘liyaenda Ela watawajibika, ili siku ya ulifi Wacheni kutikatika, kotekote mukiranda Mwakutaka kusifika, wafuasi mwawawinda Mwashinda kunung’unika, na mambo munayapinda Ishara ya kutishika, ili siku ya Ulifi Kama ni kutakasika, ni heri mkatuenenda Ghofira mkatutaka, tukawapa tukipenda Mumwombe Mahuluka, faraja akawatenda Badala ya kutimuka, ili siku ya ulifi Hitaaihirishika, siku ya ndege kupanda Mkayajibu mashtaka, ya zenu ila...