Faradhi leo n’kasema, nikapasue mbarika
asilani sitonyama’, kinaganaga ntatamka
nikosoe alosema, yake malenga wa nyika
Unisikize kwa wema, lau uje utalimka
Walau utalimuka, ukajue la kusema
Ushairi si kutamka,unagharimu taluma
Si majambo kuweka, na watu kuyasoma
Tungo zinayo mipaka, na ufundi wa kufuma
Ufundi wa kuzifuma, kwa vina muafaka
Kuviweka na vya ngama’, na tamati ukifika
Viwe na urari mwema, na utamu wa kusomeka
Msuko na mandhuma, usita na kadhalika
Si mwisho kadhalika, kuna nyingi nikusema
Mtiririko kutirika, ‘sita na kifunganyama
Ndo tungo za kusomeka, si zile unazosema
Arudhi ni ufundi kaka, wa kwongoa na mtima
Kuuongoa mtima, lazima kumakinika
Kubambanya si kwema, tungo ukiziandika
Vue ni ja kuangema, kuchelea kwajibika
Na kwogopa gharama, na mwia wa kuandika
Comments