Skip to main content

Tatasi za mtima


Kama unamjua jamani,
Kanisailie kwa nini
Mbona na mimi haneni,
na mwendoye sina sinani
Nachotaka ni hisani,
walahi sina kisirani
Nataka awe mwendani,
iwapo n'tapawa idhini

Zangu n’tetesi za mtima,
zan’tatiza hadi kusema
zanipa nyingi nakama,
na kupoka yangu naima
Anavyofanya si vyema,
kamuelezeni kwa hima
Kwamba ninaaengema,
na inaniisha neema

Kama ujumbe metuma,
ni kama kadinda kusoma
Kama sivyo angesema,
pengine naye akatuma
Kwa tuo ningesoma,
niyajue anayosema
Nijue kama ni kwema,
‘kajiamulie mapema

Nimeamba yote Nzisa,
sinayo mengine kwa sasa
lau kije kuwa kisa,
niliyemtaka nikakosa
Wala sinambe siasa,
ninaatilika kabisa
Ukimuona angusa,
na usiipoteze ruksa

Umwambie aitike,
si vyema akaniteleke,
Kwenye laini umweke,
ulainishe moyo wake
Macho yake afunguke,
na mtima wake uamke
Akubali miye wake,
aliye laazizi wake

N’ mema yenu maitiko,
ni heri kusema kuliko
Ila hayan’tui mtwiko,
wala yakanipa kiteko
Kan’tafutie aliko,
kamweleze hapa niliko
Sinacho mimi kicheko,
ni machozi ya mtiririko

Kweli hun’pati Rahabu,
unahitaji na hesabu
Kuyajua haya babu,
nimuambiayo habubu
Alejigeuza bubu,
hasikii wala hajibu
nafuu ja angejibu,
hata kwa ishara ni jibu

Haoni nivyostahabu,
na kungoja kama bawabu
Angaa nipate jibu,
jawabu litalonitibu,
H’jui kiburi harabu,
huua wala hakitibu
Hivyo mwambie sababu,
na kiini cha kunijibu

Comments

wamalwa said…
sanaa inaishi ati

Popular posts from this blog

Mja hafi kupenda

Hapana mja duniani, apenda aondowe Si khiari asilani, rohoye aitowe Aingiye pa gizani, kusiko na mwendowe Maja hafi kupenda, n’ kudura itimiye Ni kudura ya Manani, alompa utuwe Hana na lake Fulani, sema akohowe Hanalo la lakini, zake ziandikiwe Mja hafi kupenda, n’kudura itimiye          Nyaka zikiwa shirini,ni jaala apawe Au aishi theneni, neema ajaliwe Mja hana kwa nini,ikiwa aitiwe Mja hafi kupenda,n’ kudura itimiye Lau ngapewa idhini, k’teuwa atakaye Ngebaki duniani, amwali ajiliye   Afurahi maishani, na wale wampendaye Mja hafi kupenda , n’kudura itimiye

Yupi mwenye haki

1.           Yupi ale mahuluki, asiye kuwa na doa Ni yupi ale na haki, asiye wa kukosoa Mja ambaye hakiuki, akawa wa kupotea Hayupo muenye haki, maki wote meondoa 2.           Yupi asiye wa kosa, mnyofu wazo nyendo, Awapo aseme sasa, akajinegee kando, Yule ale jitakasa, safi hanao uvundo Hakuna asiyekosa, kwa kauli na matendo 3.           Sijaona aliyejitosha, akahimili nafsiye Insi asejikunguisha, ulimi kwa kauliye Nani asiye keresha, kubughudhi muumbaye Ila tu akajikosha, akatubia dhambiye 4.           Nani asiyekunguwaa, kwa fikra ya moyoni Kunaye asiye na waa, lilofichama wazoni? Awe mja anayefaa, kwa Rabana machoni? Wote wamepunguwaa, utukufu hawaoni.   5.           Yupi basi wa kupona? amchaye Mola wake Nani ataka...