Skip to main content

Kwa kuwa nakupenda


‘Meandika nikujibu, ulouliza mwenzangu
Kwelezeto nastahabu, welewe kauli yangu
Kupenda nini sababu, umenisaili tangu
Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda

Na maadamu hu bubu, utashiba jibu langu
Kukupenda si ajabu, wan’saliti moyo wangu
Mapenzi yaliusibu, kaubwaga wangu wangu
Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda

Wala sinistaajabu, hikuwa kupenda kwangu
Ngejua huba lan’karibu, ngelikaa ange kwa rungu
Likija nilidhurubu, lisitwae mtima wangu
Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda

Navyokupenda habubu, hujapendwa vile tangu
Kwangu uli kama shabu, kunitakasa uchungu
Kan’ridhie nawe hebu, ukubalie hayangu
Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda

Hukuwazia ghalibu, fikra tele kwa mafungu
Kitamani un’karibu, niwe wako uwe wangu
Viate vyako ‘sababu, vilok’zinga ja magugu
Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda

Hujui ngapi hesabu, n’mejipinda  pali mvungu
N’kililia lako jibu, litalon’toa kiwingu
Uwele likanitibu, mato yaone uwengu
Sikupendi kwa kupenda, ni kwa kuwa nakupenda

Haya ukayaratibu, nilosema kwa vifungu
Uhitimu na kutubu, ukutoke na ukungu
Huu ulokurakibu, unione mwenzangu
Kwani s’pendi tu kupenda, ila kweli nakupenda

                                                                                                                                                                                   

Comments

Popular posts from this blog

Mja hafi kupenda

Hapana mja duniani, apenda aondowe Si khiari asilani, rohoye aitowe Aingiye pa gizani, kusiko na mwendowe Maja hafi kupenda, n’ kudura itimiye Ni kudura ya Manani, alompa utuwe Hana na lake Fulani, sema akohowe Hanalo la lakini, zake ziandikiwe Mja hafi kupenda, n’kudura itimiye          Nyaka zikiwa shirini,ni jaala apawe Au aishi theneni, neema ajaliwe Mja hana kwa nini,ikiwa aitiwe Mja hafi kupenda,n’ kudura itimiye Lau ngapewa idhini, k’teuwa atakaye Ngebaki duniani, amwali ajiliye   Afurahi maishani, na wale wampendaye Mja hafi kupenda , n’kudura itimiye

Yupi mwenye haki

1.           Yupi ale mahuluki, asiye kuwa na doa Ni yupi ale na haki, asiye wa kukosoa Mja ambaye hakiuki, akawa wa kupotea Hayupo muenye haki, maki wote meondoa 2.           Yupi asiye wa kosa, mnyofu wazo nyendo, Awapo aseme sasa, akajinegee kando, Yule ale jitakasa, safi hanao uvundo Hakuna asiyekosa, kwa kauli na matendo 3.           Sijaona aliyejitosha, akahimili nafsiye Insi asejikunguisha, ulimi kwa kauliye Nani asiye keresha, kubughudhi muumbaye Ila tu akajikosha, akatubia dhambiye 4.           Nani asiyekunguwaa, kwa fikra ya moyoni Kunaye asiye na waa, lilofichama wazoni? Awe mja anayefaa, kwa Rabana machoni? Wote wamepunguwaa, utukufu hawaoni.   5.           Yupi basi wa kupona? amchaye Mola wake Nani ataka...